Jumatano 19 Agosti 2026 - 13:11
Kuanzisha Mahusiano ya Kawaida na Israel Haiwezekani na Ni Tishio kwa Uwepo wa Lebanon

Hawza/ Katika juhudi za kufungua nafasi ya kitaifa na jumuishi inayovuka tofauti za kimadhehebu na kidini, ulifanyika Mkutano wa Pamoja kwa Ajili ya Ubinadamu nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Katika juhudi za kufungua nafasi ya kitaifa na jumuishi inayovuka tofauti za kimadhehebu na kidini, na katika kipindi ambacho Lebanon inapitia, huku mashambulizi ya Kizayuni yakiendelea na kukiwa na haja inayoongezeka ya mazungumzo, kuishi pamoja na mshikamano wa Walebanon dhidi ya uvamizi, pamoja na kufufua maadili ya pamoja ya kibinadamu na kitaifa ya Walebanon, “Mkutano wa Pamoja kwa Ajili ya Ubinadamu nchini Lebanon” ulitoa “Hati ya Msingi” ya mkutano huo katika mkutano wa waandishi wa habari uliojaa hamasa katika Chama cha Waandishi wa Habari.

Dkt. Bassam al-Hashim, mtafiti na mwanaharakati wa kisiasa na mwenyekiti wa mkutano huo, katika mahojiano na “Al-Ahed”, alizungumza kuhusu malengo na mtazamo wa mkutano huo unaozingatia mazungumzo, akisisitiza kwamba mkutano huo unalenga kufufua maadili ya pamoja ya Walebanon na kuimarisha utambulisho wa kitaifa na kibinadamu unaowajumuisha wote.

Al-Hashim alisema: “Kuna ugonjwa nchini Lebanon unaoitwa ‘utambulisho wa kimadhehebu na kidini’. Kila kitu katika nchi hii kimejengwa juu yake, na mfumo huu umekita mizizi kiasi kwamba upo katika mfumo wa kisiasa, kijamii na kielimu, kwa sababu mfumo mzima umejengwa juu ya misingi ya ukabila wa kimadhehebu.”

Kwa hiyo, alisema, ni lazima tufanye kazi ya kuimarisha uelewa kuhusu utambulisho unaowakusanya pamoja Walebanon na utambulisho wa kibinadamu unaotuunganisha sote. Kwa mfano, ikiwa raia ataona kwamba kusini inaharibiwa na adui na kwamba Walebanon wanauawa kishahidi, lakini akatenda kana kwamba jambo hilo halimhusu, hilo ni tatizo kubwa.

Aliuliza: “Tumefikaje katika hali ambayo raia wa Lebanon anakuwa asiyejali kinachowapata raia wenzake?”

Kwa mujibu wa Al-Hashim, mgawanyiko huu ambao tunaishi ndani yake unamnufaisha adui na unakwenda kinyume na maslahi ya nchi na uhuru wetu. Kwa hiyo, ni lazima tufanye kila linalohitajika ili kuimarisha uelewa kuhusu utambulisho wetu wa pamoja, na juu ya yote, utambulisho wa kibinadamu. Alirejelea pia, watu walioitikia mwaliko wa mkutano huo wa kuwasiliana na kushirikiana, walikuwa wametoka katika rangi, mielekeo na misimamo mbalimbali ya kimadhehebu na kidini.

Mkutano huu una ujumbe gani?

Al-Hashim alisisitiza: Mkutano huu ni mfumo wa kielimu, kitaifa na huru unaofanya kazi ya kuchunguza na kuangazia masuala ya kitaifa, kijamii na kibinadamu nchini Lebanon. Unatoa mipango, mitazamo na mapendekezo yanayosaidia kuilinda nchi dhidi ya aina mbalimbali za hatari, kuhifadhi uhuru wake, kutetea mamlaka yake juu ya ardhi yake yote na kulinda utu wa mwanadamu ndani yake; wakati huo huo ukiimarisha amani ya ndani, maadili ya uraia na ushirikiano wa kitaifa.

Aliongeza: Tunafanya kazi ya kuchunguza kwa njia ya kielimu, yenye malengo na yenye kujenga masuala ya kitaifa na kibinadamu nchini Lebanon. Tunashughulikia changamoto zinazokabili uhifadhi wa nchi, uhuru wake na mamlaka yake, kuimarisha ujenzi wa dola yenye nguvu na yenye haki, na kuweka misingi ya utu na usalama wa mwanadamu ndani yake. Pia tunapendekeza suluhisho na mitazamo inayofaa.

Mkutano huo unalenga mshikamano wenye uwajibikaji na wahanga wa vita ambao mateso yao yanaendelea, pamoja na juhudi za kuwasaidia ili kuhifadhi haki zao zote na utu wao katika ardhi na nchi yao.

Kwa mujibu wake, kazi hii itafanywa kupitia shughuli za kiakili, utafiti, mazungumzo na pia mawasiliano yenye uwajibikaji na pande mbalimbali zinazohusika, wakiwemo taasisi na watu binafsi.

Mkutano utafanya hatua gani za kivitendo?

Al-Hashim alisema: Tumeainisha zana za kazi, kwa sasa tunaandaa masuala ya kibinadamu na yale yanayowakusanya pamoja Walebanon, na tunafanya kazi ya kufafanua “utambulisho wa kitaifa” ambao ni kiungo cha pamoja kati ya wote, pamoja na kurejesha uelewa kuhusu utambulisho huu jumuishi.

Miongoni mwa nyenzo ambazo mkutano utaxifanyia kazi ni kuchapisha taarifa, ripoti na tafiti za mara kwa mara; kuunda kamati za kielimu na vikundi maalumu vya kazi; kuanzisha majukwaa ya mazungumzo, fikra na vyombo vya habari; kushirikiana na vyuo vikuu, vituo vya utafiti na taasisi za kiraia ili kufikia malengo yaliyowekwa; na kuandaa kumbukumbu ya kitaifa yenye nyaraka kuhusu masuala, tafiti na mipango inayohusiana na hayo. Aidha, ushiriki wa wanawake na vijana wa Lebanon katika kutekeleza majukumu haya utahimizwa.

Al-Hashim alieleza kuhusu shughuli za utekelezaji za mkutano huo, akisema: Mkutano utafanya kazi ya kuandaa makongamano maalumu kuhusu masuala ya nchi na mwanadamu nchini Lebanon, hususan kuimarisha ujenzi wa dola yenye nguvu na yenye haki ya kiraia, pamoja na taasisi zake zote kwa mujibu wa Katiba; kutetea mipaka na usalama wa nchi; ujenzi upya; maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira; kurejea wakimbizi katika vijiji na miji yao katika maeneo yote ya nchi; pamoja na kuimarisha kila kinachohitajika kwa kazi hii, ikiwemo mipango, juhudi na rasilimali watu na mali, na kuwekeza utajiri na rasilimali asilia za Lebanon kwa namna inayolingana na maslahi mapana ya kitaifa.

Ni misingi gani ya kitaifa ya mkutano huu?

Katika muktadha huo, mwanachama wa “Kikao cha Watu Huru kwa Ajili ya Lebanon” alieleza kwamba; mkutano huo unaamini kuwa Lebanon ni nchi ya mwisho na ya kudumu kwa wanawe wote wa kiume na wa kike, ndani ya mipaka rasmi iliyoainishwa katika Katiba yake na inayotambuliwa kimataifa.

Alisema: Tunasisitiza umoja wa Lebanon kwa upande wa ardhi, watu na taasisi, na tunakataa aina yoyote ya uvamizi, mgawanyiko, kuchochea mifarakano, utegemezi au kudhoofisha nchi ambayo inaweza kukabiliwa nayo.

Tumejitolea kikamilifu kwa mamlaka ya kitaifa, na hatuachi hata shibiri moja ya ardhi ya nchi yetu wala haki yoyote miongoni mwa haki zake katika ardhi na mamlaka yake kamili juu yake.

Mkutano huu una msimamo gani kuhusu “kuanzisha mahusiano ya kawaida na Israel”?

Al-Hashim alisisitiza: Adui wa Kizayuni anataka kutufuta sisi kama nchi na taifa. Basi, tunawezaje kuanzisha mahusiano ya kawaida na utawala unaotaka kuiangamiza na kuikalia ardhi yetu? Na tunawezaje kufanya hali ya kawaida na adui pamoja na dhana zake za Kitalmudi zinazolenga kutufuta?

Kuanzisha mahusiano ya kawaida haiwezekani, kwa mtazamo wetu, suala la kuanzisha mahusiano ya kawaida na utawala wa Kizayuni haliwezekani.

Katika suala hili, anaamini kwamba viongozi wa Lebanon “wamejivua nguo” [wamekuwa bila ulinzi], na hivyo tunakabiliwa na wajibu wa kitaifa mbele ya miradi hii. Al-Hashim alisisitiza: Mkutano huu unamuunga mkono kila mtu anayebeba silaha kwa ajili ya kutetea uhai wa kitaifa na mamlaka yake, na unaunga mkono Jeshi la Lebanon.

Alisisitiza pia umuhimu wa kufichua masuala yanayohusiana na kuanzisha mahusiano ya kawaida na Israel, akiamini kwamba suala hili halipaswi kubaki katika kiwango cha maneno pekee, bali linapaswa kuthibitishwa na kuwekwa katika nyaraka, na kila linalohitajika lifanywe ili kufichua miradi ya siri inayolenga kuanzisha mahusiano ya kawaida na Israel.

Al-Hashim alimalizia kwa kusema: Mwishowe, “Mkutano Pamoja… kwa Ajili ya Ubinadamu nchini Lebanon” umetokana na mtazamo wa kitaifa, kibinadamu, huru na jumuishi, na unaamini kwamba kuilinda nchi, kumlinda mwanadamu na kuimarisha umoja wa kitaifa ni jukumu la pamoja linalohitaji kuunganisha juhudi za kielimu, kiakili na kitaifa, na kufanya kazi ya kuimarisha uelewa kuhusu utambulisho wa kitaifa na kibinadamu unaowaunganisha Walebanon.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha